December 06, 2014

  • SERIKALI YAPOKEA VIFAA VYA TIBA TOKA MISRI


    SERIKALI YAPOKEA VIFAA VYA TIBA TOKA MISRI
    Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imepokea msaada wa mashine nne za kusafishia damu pamoja na vifaa tiba kutoka Serikali  ya Misri, zenye thamani ya Dola Milioni 1.5.



    Mashine hizo zitatumika katika Hospitali ya Tiafa Muhimbili kwa ajili ya wagonjwa wa figo, zitaongeza uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa figo,  kwani awali mashine za kusafishia damu katika hospitali hiyo zilikuwa 15 huku zikiwa na uwezo wa kuhudumia wagojwa 60.  

    Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wakupokea msaada huo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.Self Rashidi, alisema asilimia 60 ya wagonjwa wa figo wanaopewa rufaa katika hospitali mbalimbali nchini ni wale waliofika daraja la tano la ugonjwa sugu wa figo ambao uhitaji huduma ya usafishaji damu.

    Alizitaja hospitali za Serikali ambazo zinazotoa huduma hiyo, kuwa ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Rufaa Mbeya.

    Alisema baadhi ya wagonjwa hao hufika wakiwa katika hali mahututi, na kutokana na hali hiyo mwezi Juni, mwaka huu, hospitali ya Muhimbili ikishirikiana na wahisani iliweka mashine moja ya usafishaji damu katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

    "Jumla ya wagonjwa 15-20 hufanyiwa matibabu ya upandikizaji wa figo nchini India  kwa udhamini wa Wizara ya afya na mpaka sasa kitengo chetu kimeweza kuhudumia zaidi ya wagonjwa 100 waliopandikizwa figo.," alisema Dk.Rashidi.

    Alisema kuwa wataalamu wa magonjwa ya figo nchini wapo 10 huku wengi wao wakiwa masomoni na kusababisha kitengo hicho kushindwa kutimiza malengo ya kuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati. 

    Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio waliyoyapata  bado idadi za mashine za kusafishia damu hazitoshi kulinganisha na mahitaji yaliopo.Pia huduma hii imekuwa na changamoto kutokana na upatikanaji wa vifaa tiba kuwa na gharama kubwa.

    Dk.Rashidi alisema msaada huo umekuja wakati muafaka kutokana na mikakati  ya Serikali kuboresha na kuimarisha huduma za afya na kitengo cha magonjwa ya figo,hivyo huduma itatolewa kwa wakati na kwa viwango vilivyokubalika.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.