December 06, 2014

  • CAG, ATAKA WANASIASA WAHESHIMU OFISI YAKE


    CAG, ATAKA WANASIASA WAHESHIMU OFISI YAKE
    MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad (pichani) aliyeapishwa juzi na Rais Jakaya Kikwete amekemea tabia ya wanasiasa na wafanyabiashara kuingilia kazi za kitaaluma, akisema kwa upande wake hatapenda kuona watu wa makundi hayo wakifanya hivyo na kusisitiza kuwa, kufanya hivyo ni kosa.



    Aliyasema hayo jana mbele ya waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini hapa.
    Alisema ofisi ya CAG na watendaji wengine watafanya kazi kwa kufuata maadili ya kazi, huku akiendelea kusisitiza wanasiasa na wafanyabishara kila mmoja aheshimu taaluma ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa faida ya nchi.
    Alifafanua kuwa iwapo kila mmoja atawajibika katika nafasi yake na kuaminiana katika shughuli za kila siku, kamwe hakutakuwa na matatizo yoyote.
    ''Matatizo ya watu binafsi yasichanganywe na shughuli za kila siku za ofisi ya CAG na wale wenye kufanya siasa na biashara pia wawajibike katika nafasi zao na ofisi yangu itafanya mambo kwa kufuata Katiba ya nchi inavyoelekeza, na sio vinginevyo," alisema Profesa Assad aliyekabidhiwa mikoba ya Ludovick Utouh aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.
    Alitumia fursa hiyo kuwaasa wahasibu na wakaguzi, akisema wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kiwango cha hali ya juu ili taaluma yao iweze kuheshimika nchini.
    Assad alisema kila mtaalamu wa fani hiyo anapaswa kujifunza mambo mapya, kwani kila kukicha teknolojia inakuwa hivyo nao wanapaswa kwenda na wakati.
    Awali akifungua Mkutano huo wa NBAA, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima aliwataka wataalamu wa uhasibu na ukaguzi kuwa wazalendo wa kweli kwa kulinda rasilimali za nchi ikiwa ni pamoja na kufuata maadili ya kazi yao bila kuyumbishwa.
    Alisema iwapo hilo litazingatiwa ana uhakika mkubwa uchumi wa nchi kukua kwani taaluma hiyo ni kiini cha matatizo yote ya ulaji fedha hivyo wanapaswa kuwajibika kikamilifu.
    Alisema baadhi wa wataalamu wa fani hiyo wanafanya kazi nzuri sana lakini wengine hawafanyi vizuri hivyo kila mmoja wao ajue kuwa fani hiyo ni muhimu kwa nchi na inafika wakati wa kupaswa kukemeana kwa wanaukiuka maadili yao.
    ''Fahari ya kazi hii ni kufanya kazi kwa kufuata maadili na si vinginevyo na nyie ni lazima mjione kuwa ni watu muhimu sana kwa maslahi ya nchi,'' alisema. Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Isaya Jairo aliwataka wataalamu hao kufanya kazi katika viwango vya kimataifa kwa maslahi ya nchi.
    Jairo alibainisha kwamba sasa Bodi hiyo itawaleta wataalamu kutoka nje kwa ajili ya mafunzo ya kazi katika sekta ya gesi na madini ili waweze kufanya shughuli hiyo kwa weledi mkubwa

  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.