Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea vifaa tiba vya upasuaji wa tezi dume na magonjwa mengine kutoka kwa Misri vyenye thamani ya Sh. milioni 850.
Mkurugenzi wa Wauguzi MNH, Agnes Mtawa, aliyasema hayo alipokuwa akipokea msaada wa vifaa hivyo, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema huduma ya upasuaji wa mfumo wa mkojo ambao kitaalamu unafahamika kuwa ni Urolojia hutolewa katika Hospitali ya MNH na Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Mtawa aliomba Serikali ya Misri kuwasomesha wataalamu katika eneo matumizi ya hadubini ili kutoa huduma za upasuaji kwa kiwango kinachotakiwa.
Mkuu wa kitengo cha upasuaji MNH, Dk. Ryuba Nyamasongoro, alisema kuwa asilimia 60 ya wagonjwa wanaohitaji upasuaji zaidi ni wenye matatizo kwenye mfumo wa mkojo.
Alisema huduma ya Urolojia ilianzishwa 2008 ikiwa chini ya Idara ya upasuaji kwa lengo la kuboresha huduma hiyo kwa wananchi, huduma ambazo kitengo hicho kinatoa ni pamoja na upasuaji wa tezi dume, kuziba kwa njia ya mkojo.
"Tunashukuru kupata vifaa hivyo kwa kuwa vitasaidia upungufu uliojitokeza kwa muda mrefu kuwa na kifaa cha kuondolea mawe kwenye figo," alisema.
Naye Mwanadiplomasia wa Ubalozi wa Misri nchini, Ahmed Rahim, alisema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutoa misaada mbalimbali ili kuendeleza uhusiano.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment