December 04, 2014

  • BINTI ALIYEONGOZA DARASA LA SABA AOZESHWA KWA SUKARI



    BINTI ALIYEONGOZA DARASA LA SABA AOZESHWA KWA SUKARI


    Mmoja wa wanafunzi walioongoza mtihani wa Taifa wa darasa la saba mwaka huu     mwenye umri wa miaka 16 kutoka wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro anadaiwa kuozwa kwa mwanaume mwenye umri wa miaka 50 baada ya wazazi wake kupewa sukari kilo mbili kama mahari.

    Kutokana na hali hiyo, Mtandao wa Kuelimisha Jamii kuhusu Ukeketaji mkoani Kilimanjaro (NAFGEM), umefanya jitihada za kumuokoa pamoja na wanafunzi wa kike wengine 15 waliotaka kufanyiwa vitendo vya ukeketaji kwa ngariba.

     Msichana huyo wa miaka 16 wa kabila la kimasai kutoka kata ya Orkolili (jina limehifadhiwa) baada ya kufaulu mtihani huo, aliozeshwa kwa mmoja wa wanaume ambaye ni wafugaji wa kabila hilo.

     Meneja Mipango wa Mtandao wa Kuelimisha Jamii kuhusu Ukeketeaji mkoani Kilimanjaro (NAFGEM), Honoratha Nasua,  alitoa taarifa za kuokolewa kwa wanafunzi hao katika kijiji cha Naibili wilayani hapa.

    "Wanafunzi 15 walikuwa wameandaliwa kwa ajili ya kukeketwa wakati wa mapumziko ya mwezi Desemba, mwaka huu na waliamriwa kuacha shule ili waozeshwe baada ya kukeketwa," alisema.

    Nasua alisema katika utafiti huo wamefanikiwa kupata orodha ya Mangariba wanaohusika katika mtandao wa ukeketaji.Alisema suala la  mwanafunzi huyo aliyeozeshwa limefikishwa katika Dawati la Jinsia la Polisi Wilaya ya Siha mkoani humo  kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi za kisheria.

    Kwa upande wake,  Mkuu wa Dawati la Ukatili wa Kijinsia mkoa wa Kilimanjaro, Grace Lyimo, alisema mwanafunzi huyo aliyeozeshwa aliokolewa baada ya polisi na maofisa wa NAFGEM kuingilia kati.

    Alisema wazazi wa wanafunzi huyo wameshiriki kudidimiza maendeleo ya mtoto wao kwa kukubali aolewe na kubuni mbinu mpya ya kukeketa watoto wachanga ili kukwepa vyombo vya dola na mkono wa wanaharakati.

    Lyimo alisema utafiti uliofanywa na NAFGEM, umebaini kuwa kata zilizoathirika zaidi kwa ukeketezaji ni Orkolili, Makiwaru, Karansi, Gararagua na Biriri.

    Hata hivyo, alisema inakuwa ngumu kudhibiti vitendo hivyo kutokana na kuingiliwa na masuala ya kisiasa kwa baadhi ya wagombea kuogopa kuchukua hatua kwa sababu ya kuogopa kukosa kura.

    Awali, wanafunzi walionusurika kukeketwa walimweleza Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Batilda Mhando aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya ya Siha,kuwa hawapo tayari kuolewa wala kufanyiwa tohara.

    Mtandao huo wa kupinga ukeketaji unaendesha shughuli zake katika wilaya hiyo ikishirikiana na Shirika la World Education kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Kimataifa Marekani (USAID) kupitia mpango wa Pamoja Tuwalee.
    CHANZO: NIPASHE


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.