July 21, 2014

  • Serikali, Wabunge waibana Kabanga Nickel



    Serikali, Wabunge waibana Kabanga Nickel
    Ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga (wa kwanza kushoto), ukimsikiliza Bw.Stephen Flewelling (aliyesimama), Mtendaji wa kampuni ya Glancore yenye leseni ya kuchimba Nickel katika eneo la Kabanga wilayani Ngara wakati walipofika katika makao makao makuu ya kampuni hiyo yaliyoko Toronto, Canada. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa (Mb.), (wa pili kushoto), Deogratias Ntukamazina (Mb.) (wa tatu kutoka kushoto), Murtaza Mangungu (Mb.) (wa nne kutoka kushoto) pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

    Serikali kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameitaka kampuni ya Glancore yenye umiliki wa leseni ya uchimbaji madini ya Nickel katika mgodi wa Kabanga kuacha kusuasua katika utekelezaji wa mradi huo.

    Hayo yalisemwa na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga wakati ulipokuwa katika makao makuu ya kampuni hiyo yaliyoko Toronto nchini Canada.

    Naibu Waziri aliwaeleza watendaji hao kuwa utekelezaji wa mradi huo wa uchimbaji madini aina ya Nickel katika eneo la Kabanga wilayani Ngara umechukua muda mrefu kuanza hivyo kuleta shaka kwa wananchi juu ya nia ya kweli ya kampuni hiyo kuanza uchimbaji wa madini hayo nchini Tanzania.

    "Wananchi walikuwa na matarajio makubwa juu ya mradi na walikuwa tayari kulipwa fidia ili kupisha ujenzi wa miundondombinu ya utekelezaji wa mradi na hawajaendeleza maeneo yao kwa muda mrefu, na serikali pia kwa upande wake iliweka mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 60 jijini Mwanza ambao pamoja na kuhudumia wananchi pia umeme huo utatumika katika kuendesha mgodi wa Nickel lakini mnachukua muda mrefu kutekeleza". Alisema Naibu Waziri.

    Agizo hilo la wabunge na Serikali limekuja baada ya Mtendaji wa kampuni ya Glancore Bw. Stephen Flewelling kuueleza ujumbe huo kwamba uchimbaji wa madini ya Nickel katika mgodi wa Kabanga unaweza kuanza kati ya mwaka 2018 na 2020.

    Bw. Fleweling alieleza kuwa katika kipindi cha hivi karibu bei ya Nickel duniani imeshuka mpaka kufikia chini ya Dola 6 za Marekani kwa pound hivyo kampuni inaona muda muafaka wa kuendeleza mradi huo haujafika hadi hapo bei ya madini itakapopanda katika soko la dunia.

    Naye Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina, aliwaambia watendaji wa kampuni ya Glancore kuwa mradi huo ulianza miaka ya 1970 ambapo kampuni mbalimbali zilikuwa zikijaribu kuwekeza kwenye mradi huo bila mafanikio hata hivyo baada ya kampuni ya Glancore kuja Tanzania wananchi wanaozunguka eneo la mradi walianza kuwa na matumaini kuwa uchimbaji wa madini hayo ungeanza na kutoa kila aina ya ushirikiano ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.

    " Watu walikuwa na matumaini lakini mwaka 2008 mradi ukawa kama umesimama na ilipofika mwaka 2010 matumaini yakarudi tena baada ya bei ya Nickel duniani kupanda na wananchi kutoka kipindi hiki waliambiwa wasilime mazao ya kudumu kwa vile watahamishwa pindi utekelezaji wa mradi utakapoanza, na serikali kwa upande wake imekuwa ikihakikisha kuwa masuala muhimu yanayohitajika kwenye mradi huo yanatekelezwa ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na upatikanaji wa umeme wa uhakika"alisema Mbunge wa Ngara.

    Mhe. Ntukamazina alieleza kuwa mwaka 2014 kampuni hiyo ya Glancore ilimpa taarifa kuwa bei ya madini ya Nickel duniani imeshuka kutokana nchi ya China ambayo ndiyo soko kubwa la Nickel kuanza kuzalisha "Nickel Pig Iron" ambayo ina matumizi sawa na Nickel jambo linalosababisha mradi huo kuchelewa na hivyo kuleta wasiwasi wa utekelezaji wa mradi huo.

    Akitoa ufafanuzi kuhusu masuala yaliyoelezwa na Naibu Waziri Kitwanga na Wabunge, Mtendaji wa kampuni ya Glancore alieleza kuwa mradi wa Kabanga haujafa kwa kuwa tayari wameshawekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 260 ila changamoto kubwa ni kushuka kwa bei ya madini ya Nickel katika soko la Dunia na kwamba bado wanaamini kuwa mradi huo una manufaa kwao na kwa Tanzania.

    "Ingawa mradi huo haujaanza kutekelezwa, mawasiliano na wananchi yanaendelea ili kutoa elimu juu ya maendeleo na hatua stahiki tunazochukua kuhusu utekelezaji wa mradi huu ili wananchi hawa wasikose matumaini katika kipindi hiki cha mpito." Alisema Bw. Flewelling.

    Kuhusu suala la wananchi wa Kabanga kuendeleza maeneo yao alieleza kuwa wananchi wameruhusiwa kuendeleza maeneo hayo mpaka hapo utekelezaji wa mradi utakapoanza rasmi na masuala ya ulipaji fidia kuanza ambapo jumla ya Dola za Marekani milioni 70 zinategemewa kutumika.

    Naye Naibu Waziri Kitwanga aliwaeleza watendaji hao kuwa serikali sasa inaangalia maendeleo ya nchi na kwamba haihitaji wawekezaji wanaoshikilia maeneo kwa muda mrefu bila kuyaendeleza hivyo inahitaji kuona eneo hilo likiendelezwa na si vinginevyo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.