July 03, 2014

  • Njama chafu za kuidhoofisha CHADEMA: ‘Tatizo ni Mbowe, Dk. Slaa’



    Njama chafu za kuidhoofisha CHADEMA: 'Tatizo ni Mbowe, Dk. Slaa'
    ILI kudhibiti nguvu ya upinzani na kujihakikishia ushindi katika uchaguzi ujao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kuwekeza katika mikakati michafu dhidi ya viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hasa Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa.

    Wachambuzi kadhaa wa mwenendo wa siasa nchini wameliambia gazeti hili jana kwamba njia ya kuihakikishia CCM ushindi mwakani ni kuhakikisha Mbowe na Dk. Slaa hawawi sehemu ya uongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.

    Kwa mujibu wa watoa habari wetu, ambao hawakupenda kutajwa gazetini, hata chokochoko za wanachama wasaliti na waliofukuzwa ambao bado wanaona fahari kujihusisha na kile wanachoita jitihada za "kusafisha CHADEMA", ni sehemu ya mkakati mzito wa CCM kutumia watu wanaoonekana kuwa ndani au karibu ya chama hicho, ili kuonyesha umma kwamba kina migogoro.

    "Imewachukua CCM muda mrefu kutambua uwezo wa Mbowe kuongoza na kupanga chama kimkakati. Kama wangejua zamani wangeshammaliza kabla hajaonyesha makali. Hata hivyo, bado wanasema wana muda, na wana vijana wanaoweza kuifanya kazi hii kwa malipo kidogo tu," alijitapa mmoja wa wachambuzi hao, akidai anajua kwa karibu mipango ya baadhi ya vigogo wa CCM.
    Alisema kwamba awali walijaribu kutumia mbinu zile zile walizotumia kuua au kudhoofisha vyama vya upinzani huko nyuma, hasa NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na Tanzania Labour Party (TLP), lakini wamegundua kuwa haziwezi kufanya kazi kwa CHADEMA kwa sababu kina viongozi wasio wepesi.

    Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, CCM walitumia ruzuku na ushushushu kama silaha ya kuua vyama kwa kupandikiza migogoro. Mahali pengine walitumia pesa, na hisia za udini, ukabila na ukanda, lakini kwa CHADEMA wamegundua hoja hizo hazina mashiko kwani chama kimekuwa kinakua kila sehemu ya nchi.

    "Kwa NCCR-Mageuzi ilikuwa rahisi kusema wanagombania ruzuku. Wakati huo ruzuku kwa vyama lilikuwa jambo jipya, na ni kauli ambayo iliaminika kirahisi. Hata pale walipoanza kushambuliana kwamba mashushushu wamevamia chama, ilikuwa rahisi kwa umma kuamini.
    "Viongozi waligombanishwa bila kujua, chama kikameguka. Mwenyekiti akaondoka na pande lake, na katibu akabaki na lake. Kwa CHADEMA imeshindikana kuwatenga mwenyekiti na katibu mkuu, hivyo chama kimebaki kimoja.

    Hata hawa walioondoka, wameondoka na makundi ya watu, lakini hayana nguvu ya kubomoa chama. Mbinu kuu iliyobaki sasa ni kuhakikisha Mbowe na Dk. Slaa wanaondoka kwenye uongozi. Hapo hutaona CHADEMA tena," alidokeza.

    Mchambuzi mwingine ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema kinachowatisha CCM ni kwamba Mbowe na Dk. Slaa hawatingishiki kwa pesa wala kwa vitisho.
    Alisema: "Hata hii mbinu ya kutumia akina Zitto imeshindwa kuleta matunda waliyotaka. Sasa hapa kuna mambo kadhaa ya kuchunguza. Tazama vijana waliokimbilia kwenye chama kipya kilichoanzishwa na kusajiliwa haraka haraka. Sikiliza lugha wanayotumia kujenga chama chao. Wanashambulia viongozi wa CHADEMA.

    "Ukitazama juhudi kubwa za kujenga na kukuza CHADEMA katika kipindi cha uongozi wa Mbowe na Dk. Slaa, utaelewa kwanini CCM na baadhi ya wasiotakia mema CHADEMA, wanawashambulia viongozi hawa kwa kishindo.

    "Kumbuka kauli na tambo za Wassira na Mwigulu kwamba CHADEMA itakufa. Wanajua kuwa CHADEMA chini ya Mbowe na Slaa haiwezi kufa. Kwa hiyo, ili ife inabidi wawili hawa waondoke, ishikiliwe na wengine ili CCM wabahatishe tena.
    "Si kwamba chama hakina watu wengine wenye uwezo, lakini ukweli ni kwamba uongozi wa Mbowe na Slaa umeijenga CHADEMA ikawa tishio ambalo CCM wasingependa kuliona likisitawi hadi uchaguzi mkuu ujao."

    Kumbukumbu zinaonyesha kwamba wakati Mbowe anapewa dhamana ya kuongoza chama hiki mwaka 2004, CHADEMA ilikuwa na wabunge wanne tu wa kuchaguliwa na mmoja wa viti maalumu. Madiwani hawakuzidi 100.

    Mwaka 2005 kilipata wabunge 11, na mwaka 2010 kilipata wabunge 49, na mamia ya madiwani. Kinaongoza mamia ya mitaa, vitongoji na vijiji. Kinazidi kuaminiwa na kupata maelfu ya wanachama. Hamasa na umaarufu wa CHADEMA vimeongezeka nchi nzima.
    Wasomi na wafanyabiashara wamezidi kujiunga na CHADEMA, ujasiri wa wananchi umeongezeka, na chama tawala kimeyumba katika maeneo mengi.

    Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba Mbowe na Slaa hawahongeki. Kwa hiyo, CCM imedhamiria kuwachonganisha na wanachama, na kuhakikisha wanaondolewa kwenye uongozi kwa mbinu zozote zile.

    Mbinu ya sasa inayotumiwa ni kutumia makundi ya waasi ndani ya CHADEMA, na waliokwishapoteza uanachama kudai kwamba Mbowe hastahili kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu.
    Wiki hii baadhi ya vyombo vya habari vilimnukuu ofisa mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa akisema maneno hayo hayo, ingawa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, John Mnyika alitoa kauli haraka haraka kupinga kauli hiyo, akisema mtoa kauli amekurupuka, na hizo ni dalili za ofisi hiyo kutumika vibaya.

    Wakati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema uongozi wa CHADEMA uliondoa kipengele cha ukomo wa muda wa uongozi bila kufuata utaratibu wa kikatiba, gazeti hili limegundua jambo tofauti.
    Mawasiliano ya kimaandishi kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama, Jaji Francis Mutungi na CHADEMA, yanaonyesha kuwa mambo yote yalifuata utaratibu.
    Kwa mujibu wa barua ya Januari 15, 2014 (Kum.Na.DA.112/123/16A/19), Msajili alidai kuwa Ibara ya 6.3.2c ya Katiba ya CHADEMA ilichomekwa kinyemela bila kupitishwa na mkutano mkuu wa chama.

    Lakini barua ya CHADEMA kwenda kwa makatibu wa wilaya na mikoa nchi nzima, Julai 13, 2006 (Kumb. C/HQ/ADM/CIR/15/139), inaeleza wazi maeneo yaliyokuwa kwenye mchakato wa kufanyiwa maboresho.

    Aya ya mwisho inasomeka hivi: "Pia pendekezo la Ibara ya 6:3.2 (c) ya rasimu inasomeka: 'Kiongozi aliyemaliza muda wake wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena, ilimradi awe ametimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi.' Badala ya Ibara ya 6:3.2 (c) iliyokuwa inaweka kikomo cha muda wa awamu mbili kwa viongozi kuwa madarakani katika cheo kimoja kwa ngazi moja ambacho kimeondolewa."
    Barua hiyo ilisainiwa na Shaibu Akwilombe aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, ambaye sasa ni katibu wa CCMMkoa wa Mtwara.

    Mwezi mmoja baadaye, Agosti 13, 2006, Mkutano Mkuu wa CHADEMA ulipitisha maboresho hayo na mengine yaliyokuwa yamependekezwa na kupitiwa na wajumbe.
    Mkanganyiko Ofisi ya Msajili

    Juzi CHADEMA ilisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilikurupuka kutoa tamko kuhusu ukomo wa viongozi wao pasipo kuzingatia kwa ukamilifu maelezo na vielelezo vilivyopelekwa kwenye ofisi yake baada ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2006.
    Tanzania Daima imeona barua nyingine, Kumb. DA/112/123/01/125, iliyosainiwa na Msajili Msaidizi Sisty Nyahoza. Inasema, "Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatoa ufafanuzi kuwa vipindi vya uongozi katika vyama vya siasa huwekwa na katiba za chama husika.
    "Msajili wa Vyama vya Siasa anaviasa vyama vya siasa kuzingatia katiba zao na si kumwomba msajili kusogeza mbele chaguzi zenu za ndani, kwani sheria haimpi msajili mamlaka hayo.

    Kwa mujibu wa barua hiyo, msajili amesema kuwa anaelewa changamoto zinazovikabili vyama vya siasa.

    chanzo: Tanzania daima

  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.