July 06, 2014

  • MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini atafuta upenyo kuwarejesha Ukawa bungeni



    MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini atafuta upenyo kuwarejesha Ukawa bungeni

    MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ameingilia kati kuondoa changamoto zilizojitokeza katika awamu ya mchakato ya Bunge Maalumu la Katiba ambalo baadhi ya wafuasi wa kundi linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wengi wakiwa viongozi wa vyama vya upinzani, walisusia.

    Aidha, walitangaza kuendelea kususia awamu ya pili ya siku 60 inayotarajiwa kuanza Agosti 5, mwaka huu, kwa kile walichodai `kumezwa' na wenzao wa chama tawala, CCM, hali iliyowashangaza wengi kwa kitendo cha kutoka nje ya Bunge ambako wangeweza kujenga hoja nzito.
    Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mutungi alisema alikutana na viongozi wa CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na kujadiliana nao kwa kina katika mambo yaliyojikita kutafuta njia ya kuondoa changamoto zilizojitokeza katika mchakato huo.

    Aliongeza kuwa msajili wa vyama vya siasa ni mlezi wa vyama vya siasa na vyama vya siasa vina sauti kubwa katika mchakato huo, hivyo ana wajibu wa kuwaita na kushauriana nao.

    Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza msimamo mpya wa Ukawa baada ya awali kusisitiza hawatarejea bungeni, licha ya kuombwa kufanya hivyo na Rais Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge, viongozi wa dini wakiwemo maaskofu na mashekhe, wanasiasa mashuhuri wa ndani na nje ya nchi, akiwemo Kiongozi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, Helen Clark aliyewataka wana-Ukawa kutumia fursa ya Bunge Maalumu la Katiba kuipa nchi Katiba bora, badala ya kuyumbisha mchakato kwa kususia vikao vyake. Clark, Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand alisema hayo akiwa nchini Mei mwaka huu.

    Aidha alisisitiza kuwa Katiba bora inaweza kupatikana kwa kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu, na kwamba kinyume cha hapo ni kudhoofisha nia njema ya Serikali ya kupatikana kwa katiba mpya.
    "Kwa maoni yangu kama ninayoyasikia ya kuwepo kwa kundi lililotoka nje ya Bunge la Katiba ni kweli, nawashauri wabadilishe msimamo; kazi ya kutunga Katiba inapaswa kuwa na wigo mpana, si wa makundi… Bunge la Katiba ni mahali pekee ambako wazalendo wa kweli wanaweza kujenga hoja nzito kwa lengo la kuhakikisha inapatikana Katiba bora," alikaririwa akisema Clark.

    Mutungi ambaye alitafutwa kwa simu ili kufafanua msimamo wa Ukawa na kukataa katakata kuzungumzia suala hilo akisema taarifa yake inajitosheleza, alisema ili kufanikisha mchakato wa kujadili rasimu ya pili ya Katiba mpya, ofisi yake haiwezi kupuuzia umuhimu wa ushiriki na uwepo wa wajumbe wote katika Bunge la Katiba ili mchakato huu uendelee kwa mafaniko yanayotarajiwa na watanzania wengi ni muhimu kuhakikisha kunatafutwa maridhiano kati ya pande zinazokinzana.

    Alisema mchakato wa kupata Katiba mpya unaelekea kukwama kutokana na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kususia vikao na shughuli za bunge hilo.
    Pia alisema katika mchakato huo, Bunge Maalum la Katiba vyama vya siasa vimeonekana kuwa na sauti kubwa, kwani hata changamoto zinazojitokeza zinasababishwa na misimamo na mitazamo ya vyama vya siasa.

    Alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa vyama vya siasa kuweka maslahi ya Taifa mbele kwa kitendo chao cha kizalendo cha kukubali kushiriki katika majadiliano.
    Pia aliwaomba wanachama wa vyama husika na Watanzania kwa ujumla kuunga mkono jitihada hizi ili ziweze kuzaa matunda ya kuwezesha kuendelea na kukamilika mchakato huu kwa amani na maridhiano yenye sura ya umoja wa kitaifa.

    UWT, TADEA Wakati Msajili wa Vyama akitaka kuhakikisha Ukawa wanarejea bungeni, Umoja wa wa Wanawake Tanzania (UWT), nao umewataka wanaounda kundi la Ukawa na wafuasi wao kurejea bungeni kuendelea na vikao vya Bunge Maalum la Katiba linalotarajiwa kuendelea kwa siku 60 kuanzia Agosti 5, mwaka huu, kwani kitendo cha kususia bunge hilo si cha kiungwana kwani azma iliyopo ni kuipatia nchi Katiba mpya.

    Kauli ya UWT imetolewa na Mwenyekiti wake wa Taifa, Sophia Simba alipokuwa anafungua kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la umoja huo.
    Alisema kitendo cha UKAWA kususia Bunge hilo maalumu pia kimekuwa kikiwatia hofu wananchi juu ya hatima ya nchi katika kupatikana kwa Katiba mpya.

    Alisema hata kama itashindikana kupatikana kwa katiba mpya bado ni muhimu kwao kurejea bungeni kwani kwa sasa nchi ina katiba inayoiongoza. Simba aliwataka wajumbe wa mkutano huo kwenda kuwafahamisha wananchi hasa wanawake kuwa wasiwe na wasiwasi juu ya amani na utulivu uliopo kwa sasa nchini.
    "Kususa si uungwana, ni kama utoto kwani Rais Jakaya Kikwete aliwateua kwa nia njema tu ni muhimu kila moja kuhakikisha Katiba mpya inapatikana," alisema.

    Aidha akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa Simba alisema wakati umefika sasa kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi hizo na kuacha kuwaachia wanaume kwa kujiona kuwa hawawezi.
    Ushauri mwingine wa aina hiyo umetoka kwa chama cha siasa cha The African Democratic Alliance Party (TADEA) ambapo jana Katibu wake Mkuu, Juma Ali Khatib alikutana na waandishi wa habari kuzungumzia umuhimu wa Bunge Maalumu la Katiba katika mchakato wa kupatikana Katiba mpya.
    Alisema ni vyema viongozi wa Ukawa na wafuasi wao wakasitisha ubishani usio na faida, zaidi ya kuchelewa mchakato wenye faida kwa kila Mtanzania.

    "Ukawa warudi bungeni watangulize Taifa kwanza na kujadili mambo ya msingi ambayo yapo na yanaweza kujadilika na kupatikana Katiba bila kuwa na migogoro," alisema Khatib.
    Hatua ya Msajili, viongozi wa vyama vya siasa, wanazuoni, viongozi wa dini na watu wenye kuitakia mema Tanzania katika mchakato wa kupata Katiba mpya inakuja baada ya kundi la Ukawa kutangaza kuendelea kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hata litakaporejea tena Agosti 5, mwaka huu kwa awamu ya pili ya mchakato wa Katiba mpya baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia kuongeza siku 60 zaidi.

    Awali, wajumbe hao walikutana kwa siku 70 kuanzia Februari 11 mwaka huu, lakini mchakato wake ulisuasua kutokana na mivutano ya mara kwa mara, hasa kutoka kundi la ukawa linaloundwa na baadhi ya viongozi wa kambi ya upinzani na wafuasi kutoka katika kundi maalumu la watu 201 walioteuliwa na Rais kwa ajili ya Bunge hilo.

    chanzo:habari leo


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.