July 03, 2014

  • ALIUZA FIGO KWA KUDHANI KUWA INGEOTA NYINGINE



    ALIUZA FIGO KWA KUDHANI KUWA INGEOTA NYINGINE
    Katika mitaa ya Jiji la Kathmandu, nchini Nepal kukutana na watu wakiomba msaada wa matibabu ya figo ni jambo la kawaida.
    Duniani kote, tatizo la figo siyo jambo geni masikioni mwa watu. Wapo wengi wanaosubiri kubadilisha na wengine kupata matibabu ya kawaida.
    Hata hivyo, kwa Nepal ni habari nyingine kabisa. Siyo kwamba watu hawa wanataka kubadilishwa figo kama wale wengine duniani ambao wana matatizo ya kawaida. Hawa hawana kwa sababu walirubuniwa na zikachukuliwa bila wao kujua.
    Hivi sasa wanaugua magonjwa mbalimbali kwa sababu hawana uwezo wa kugharimia matibabu ya figo (dialysis) kutokana na umaskini uliotopea.

    Inakadiriwa kuwa watu wapatao 300 katika kipindi cha miaka mitano, wameingia katika mtego wa wafanyabiashara wa figo na wamezitoa bila wao kujua.
    Mwathirika wa biashara hiyo, Nawaraj Pariyar anasimulia jinsi alivyodanganywa kuwa nyama wanayoitoa tumboni mwake ingeota tena bila kujua kinachotolewa ni figo.
    Kama walivyo wakazi wengi nchini humo, Pariyar naye alikuwa akiishi kwa kutegemea biashara ya maziwa kutoka katika ng'ombe wawili anaowamiliki.
    Pariyar ni maskini ambaye hakwenda shule hata darasa moja, mbali na kumiliki ng'ombe hao. Analo shamba dogo ambalo halimtoshelezi kulima mazao yatakayompa chakula cha angalau kwa miezi sita.
    Katika kujiongezea kipato, alikuwa akienda mji mkuu wa nchi hiyo, Kathmandu kutafuta vibarua vya ujenzi.
    Akiwa katika moja ya vibarua hivyo mwaka 2005, kiongozi wa ujenzi katika jengo alilokuwa akifanya kibarua alimfuata kumpa 'mchongo' ambao ungemfanya apate chapchap Dola 30,000 za Kimarekani 30,000.
    "Aliniambia kuna kipande cha nyama kitatolewa tumboni nami nitapewa kiasi hicho cha pesa. Nilipotaka kuhoji zaidi aliniambia nisiwe na wasiwasi kwani kipande hicho kitaota tena baada ya muda," anasema Pariyar.
    "Nilifikiria kama nyama itaota tena kwa nini nisikubali tena ninapata pesa nyingi kiasi hicho."
    Anasema kabla ya kukubaliana naye alimuuliza itakuaje kama atakufa wakati wa kuitoa nyama hiyo, lakini alimhakikishia kuwa itatolewa na wataalamu waliobobea hivyo asiwe na wasiwasi.
    Anasema maisha yalibadilika kuanzia pale alipokubali kwani alipewa nguo nzuri na chakula. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake alipelekwa katika jumba la sinema.
    Wahalifu hao walimpeleka katika hospitali moja nchini India katika mji wa Chennai.
    "Tulipofika hospitali daktari aliniuliza kama nina undugu na mgonjwa, nilikubali kwa kuwa ndivyo nilivyoambiwa niseme," anasema Pariyar.
    "Nilisikia mara kadhaa wakisema kidney (figo) lakini sikuelewa kwa sababu katika lugha yetu huwa inaitwa mirgaula," anaongeza.
    Anasema kama angejua kama kinachozungumziwa ni figo, asingekubali kuendelea na zoezi hilo.
    Baada ya kutolewa figo, Pariyar aliondolewa na kurudishwa kwao huku akiambulia Rupee 20,000 tu ambazo hazifikii hata robo ya makubaliano yao.
    "Baada ya muda nilipata wasiwasi. Nikaamua kurudi kwa daktari kuulizia kwa sababu hata wale watu sikuwaona tena, ndipo nilipogundua kuwa figo yangu imechukuliwa," anasema Pariyar.
    Hivi sasa Pariyar anaugua mara kwa mara. Ana matatizo katika mkojo na mgongo unamuuma mara kwa mara.
    "Najua nitakufa hivi karibuni. Natumaini nikifa leo Serikali itanisaidia kuwatunza watoto wangu wawili. Sijui kama nitakufa leo au kesho lakini siku zangu zinahesabika," anamalizia.
    Wito wake kwa serikali ya nchi hiyo ni kuwaelimisha wananchi wake ili wasirubuniwe kwa sababu ya umaskini wao na kukosa elimu.
    Kwa mwaka jana pekee, watu 10 walikamatwa katika majaribio ya kutaka kuwasafirisha watu ili wakawatoe figo na kuziuza.
    Chanzo:Mwananchi


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.