July 06, 2014

  • WANANCHI WILAYANI KIBAHA WAPATIWA MAJI BURE



    WANANCHI WILAYANI KIBAHA WAPATIWA MAJI BURE
    Na John Gagarini, Kibaha

    WAKAZI wa Mitaa ya Vikawe, Vikawe Shuleni, Vikawe Bondeni na Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wamepatiwa ofa ya kutumia maji bure kwa miezi mitatu baada ya huduma hiyo kuanza kupatikana ambapo mitaa hiyo haikuwa na maji ya bomba tangu kuanzishwa kwake.

    Maji hayo tayari yameshaanza kutoka yanatokana na chanzo cha maji cha Ruvu Juu baada ya mitaa hiyo kutokuwa na maji kabisa ambapo awali walikuwa wakitumia maji ya visima na mto .

    Akizungumza na mabalozi, makatibu na viongozi wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mkuza wilayani Kibaha wakati wa semina ya viongozi hao iliyofanyika jana mjini Kibaha, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Silvestry Koka alisema kuwa maji yameanza kutoka kwenye mitaa hiyo hivi karibuni.

    "Wananchi hao wamepata ofa hiyo ya kutumia maji bure lakini baada ya miezi mitatu wataanza kuyalipia maji hayo baada ya kukosa maji ya bomba kwani kulikuwa hakuna maji kabisa na walikuwa wakichota maji kwenye visima na mto ambapo baadhi walipoteza maisha kwa kukamatwa na mamba walipokuwa wakichota maji mtoni," alisema Koka.

    Katika hatua nyingine Koka alisema kuwa mji wa Kibaha utaondokana na tatizo kubwa la ukosefu wa maji baada ya mradi wa bomba kubwa kutoka chanzo cha mto Ruvu kuanza.

    Koka alisema kuwa kwa muda mrefu wa mji huo umekuwa ukikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji huku wakati mwingine maji yakiwa yanatoka kwa mgao kutokana na chanzo kilichopo kutokuwa na uwezo wa kutoa maji ya kutosha.

    "Mradi huu kwa sasa uko kwenye hatua nzuri ambapo uchimbaji wa mtaro utaanza muda wowote kuanzia sasa kwani taratibu zingine zimekamilika na bomba litakalopitishwa litakuwa ni kubwa ambalo litapitisha maji mengi," alisema Koka.

    Kwa upande wake katibu wa (CCM) Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni utekelezaji wa ilani ya chama ambayo ni ahadi kwa wananchi ili kuboresha utoaji huduma.

    Mdimu alisema kuwa chama kupitia kwa viongozi wake kitahakikisha ahadi zote zinatekelezwa kwa wakati uliopangwa ili wananchi waondokane na kero za huduma muhimu.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.