July 13, 2014

  • Wajasiriamali nchini kujengewa uwezo zaidi-Dr Nagu



    Wajasiriamali nchini kujengewa uwezo zaidi-Dr Nagu
    SERIKALI kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), itaendelea kutoa mafunzo ya wafanyabiashara wadogo na wakati (SMEs) ilikuboresha zaidi mahusiano ya kibiashara na wafanyabishara wakubwa na makampuni.
    Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji),Dkt. Mary Nagu, alisema jijini Dar es Salaam hivi karibu kuwa tayari wajasiriamali  214 wameshafaidika na mafunzo hayo hapa nchini. Miongoni mwa walionufaika 152 ni wanaume na 62 ni wanawake.
    "Kupitia mafunzo haya, wajasiriamali wadogo na wakati wataunganishwa na makampuni makubwa katika sekata za mawasiliano, ujenzi, kilimo, saruji, madini,viwanda vya samaki, bia, viwanywaji baridi na hoteli," alisema waziri Nagu.
    Kwa mujibu wa Dkt. Nagu, Mafunzo hayo yanayojulikana kama 'Business Linkage' yana umuhimu mkubwa wa kuboresha mahusiano ya kibiashara katika wajasiriamali wadogo na wakati na wafanyabiashara wakubwa/makampuni.
     "Sisi kama serkali, tumedhamiria kwa dhati kuisaidia zaidi kada ya wajasiriamali wadogo na wakati kukua na kuiwezesha kuchangia ipasavya katika ukuaji wa uchumi wetu wa taifa," aliongeza.
    Waziri Nagu alisema mafunzo hayo yameshafanyika Dar es Salaam, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro), na Kanda ya Ziwa(Mwanza).
    Akifafanua zaidi kuhusu mafunzo hayo ya kuboresha mahusiaono ya kibiashara,wafanyabiashara/wasambazaji 54 walihitimu mafunzo ya usambazaji bidhaa za ndani(Local Suppliers) sawa na asilimia  85.3.
    "Tayari tafiti zilizokwisha fanywa kwa wajasiriamali ambao wameshapata mafanzo zinaonyesha kuwa mpaka sasa wanafanya vizuri sana katika biashara zao," alisisitiza waziri Nagu na kuelezea umuhimu wa mafunzo kama hayo kwa wajasiriamali.
     Kwa upande mwingine, Waziri Nagu alisema kuwa TIC ilishatembelea jumla ya miradi 99 ya wawekezaji na kutoa huduma bora (Aftercare Services) na kujenga mahusiano mazuri na wawekezaji hapa nchini.
     "Ziara hizi ambazo zimeshafanywa sehemu mbalimabali hapa nchini zilikuwa za manufaa makubwa kwani zilitoa fursa kwa kituo kusikiliza kero wanazozipata wawekezaji na kuzifikisha sehemu husika kwa ufumbuzi," aliongeza.
    Waziri huyo mwemye dhamana ya uwekezaji na uwezeshaji, alisema kuwa serikali ya Awamu ya Nne nchini ya Dkt. Jakaya Kikwete imefanya mageuzi makubwa katika nyanja za uwekezaji hapa nchini na bado inafanya jitihada zaidi katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza.
     Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Biashara na Maendeleo (UNCTAD), mwaka 2013,Tanzania ilikuwa na mitaji toka nje yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 12.7 ikiipita Kenya iliyokuwa na dola bilioni 3.4 na Uganda dola bilioni 8.8.

    Kwa mujibu wa takwimu hizo, kwa mwaka 2013 Tanzania peke yake ilivutia mitaji ya uwekezaji toka nje yenye thamani ya dola bilioni 1.9 na kuipita mbali Kenya iliyovutia dola milioni 514 katika kipindi hicho.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.