July 03, 2014

  • TPDC yaibuka kidedea kwenye maonesho ya Sabasaba


    TPDC yaibuka kidedea kwenye maonesho ya Sabasaba
    Greyson Mwase na Malik Munisi

    Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) limeibuka kidedea na kukabidhiwa kikombe cha ushindi katika kundi la mashirika ya petroli na mafuta nchini baada ya kuyabwaga chini mashirika megine mengi yaliyokuwa yanawania kikombe hicho katika maonesho ya kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo jijini Dar es Salaam.

    Kikombe hicho kilikabidhiwa na mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ambapo aliyataka makampuni mengine kuiga mfano wa TPDC katika uwekezaji kwa maendeleo ya nchi.

    Balozi Iddi alisema ili nchi yoyote iweze kukua kiuchumi haina budi kuwekeza kupitia viwada na kusema kuwa serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa viwanda vinachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

    Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kikombe hicho kwa niaba ya TPDC msemaji wa shirika hilo na msimamizi wa banda Bw. Sebastian Shana amesema kuwa ushindi huo ni faraja kuwa kwa shirika hilo na kuongeza kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia sekta za gesi na mafuta.

    Akizungumzia siri ya mafanikio ya ushindi kwa shirika la TPDC Bw. Shana alisema kuwa ni kuanza maandalizi mapema na kujituma zaidi hali iliyopelekea shirika hilo kufanya vizuri zaidi.

    Akizungumzia mikakati ya shirika hilo Bw. Shana alisema kuwa shirika hilo limepanga kufanya utafiti zaidi wa gesi na mafuta kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa kiuchumi.

    " Unajua nia ya serikali ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa katika kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, na katika kuhakikisha serikali inafikia lengo hilo, TPDC ipo tayari kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kuendeleza sekta ya gesi na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi." Alisema Bw. Shana.

    Bwana Shana aliendelea kusema kuwa gesi iliyogunduliwa inachangia kwa zaidi ya asilimia 50 katika umeme wa gridi ya taifa na kusisitiza kuwa kama shirika, wako tayari kuweka nguvu zaidi katika utafutaji na uzalishaji wa gesi ili iweze kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uzalishaji wa umeme.

    Bw. Shana alisema kuwa TPDC imekuwa ikishirikiana na wadau wakuu kama Wizara ya Nishati na Madini ambayo imelisaidia shirika hilo kupiga hatua kubwa katika uendelezaji wa shughuli za utafutaji wa gesi na mafuta.

    Hii ni mara ya saba kwa shirika hilo kujinyakulia vikombe kwenye maonesho ya kimataifa ya Sabasaba tangu lilipoanza kushiriki.
    Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Saif Ali Idd akifungua maonesho ya kimataifa ya Saba Saba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
    Mtaalam kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) Bi. Edith Simtengu akipokea kikombe cha ushindi kwa niaba ya washiriki wenzake.
    Washiriki kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) wakiwa katika picha ya pamoja na kikombe cha ushindi mara baada ya kuibuka washindi wa kwanza katika kundi la makampuni ya mafuta na gesi katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam
    Mtaalam kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) Bw. Emmanuel Gilbert akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda hilo kwenye maonesho ya kimataifa ya Saba Saba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.