July 13, 2014

  • Rais Kikwete: Uchaguzi Serikali za Mitaa kusogezwa mbele




    Rais Kikwete: Uchaguzi Serikali za Mitaa kusogezwa mbele

    RAIS Jakaya Kikwete amesema uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulikuwa ufanyike mwezi Oktoba mwaka huu, huenda ukasogezwa mbele kutokana na kutokamilika kwa mchakato wa rasimu ya mabadiliko ya Katiba.
     
    Kauli hiyo ameitoa kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Tanga.
     
    Alisema kulingana na hali ilivyo hivi sasa ambapo Bunge la Katiba halijakamilisha kazi zake, ni dhahiri kwamba uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi huo kwa kutumia Katiba mpya haupo.
     
    "Kwa mfano, wabunge endapo wataamua wapitishe kwamba katiba itambue serikali 3 ni lazima kwanza itungwe katiba ya Tanganyika ambayo itaainisha taratibu zitakazotoa mwongozo wa uchaguzi…hata kama itabaki kama ilivyo …. bado muda wa kuandaa huo utaratibu wa uchaguzi wa serikali za mitaa hautatosha kwa sasa", alisema.
     
    Aidha aliongeza, "Nimeona niliseme hili japo kwa ufupi kwamba uchaguzi huu huenda utalazimika kusogezwa mbele kutokana na kutokamilika kwa mchakato wa Rasimu ya mabadiliko ya Katiba", alisema.
     
    Katika hatua nyingine, Rais amewataka Maofisa Kilimo kwenye halmashauri kujiendeleza kitaaluma na kuwa mabingwa waliojikita katika taaluma ya mazao yanayostawi kwenye maeneo yao badala ya kuyashughulikia kwa ujumla mazao yote yanayolimwa na wananchi.
     
    Alisema utekelezaji wa agizo hilo utaongeza mavuno kwa zao husika, utapanua wigo wa uzalishaji pamoja na utaalamu katika kushughulikia zao, aina ya zao na kuleta tija katika sekta ya kilimo.
     
    Alisema hatua ya maofisa kilimo kuendelea kujishughulisha kwa ujumla na mazao yote yanayostawi bila kuwa na lengo la kusimamia mazao maalumu, kunaifanya sekta hiyo kudumaa na hivyo kushindwa kuwakwamua kiuchumi wananchi.
     
    "Nimegundua kwamba watu wetu wengi hawana utaalamu uliobobea…hata maofisa kilimo wetu hawana taaluma maalumu zilizojikita kwenye aina ya mazao mengine zaidi ya mpunga na mahindi, hatua ambayo inawasababisha washindwe kusimamia vizuri uzalishaji wa mazao mengine ambayo yangeweza kuwakwamua kiuchumi wakulima kwenye halmashauri husika," alisema.
     
    Aliongeza, "Kwa hiyo ni jukumu lenu viongozi wa halmashauri kuwachukua maofisa kilimo wenu na kuwapeleka SUA kwa ajili ya ku-specialize (kujikita) kulingana na vipaumbele vyenu vya mazao kwa sababu sio wote wanao ubingwa katika kila zao…tukifanikiwa kwenye hilo tutapata mafanikio zaidi", alisema.
     
    Aidha aliwataka viongozi kwenye mkoa wa Tanga kuhakikisha shughuli za kilimo zinajikita kwenye uzalishaji endelevu wa mazao ya matunda na mboga, kwa kuwa mkoa huo uko katika fursa nzuri kiuzalishaji zaidi ya mazao ya nafaka.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.