Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi akizungumza wakati wa Mkutano wa Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa iliyokuwa ikijadili ajenda kuhusu tathmini ya jumla ya Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi zinazochangia wanajeshi wake katika operesheni hizo za ulinzi wa amani.
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wakifuatilia majadiliano ya ajenda kuhusu Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa ya kuwa itaendelea kushirikiana na wapenda amani katika kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC) kuwa na amani na usalama.
Akichangia majadiliano juu ya ajenda inayohusu tathimini ya jumla ya Operesheni za Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa. Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi amesema, Tanzania inafanya hivyo kwa kutambua wajibu wake katika medani ujenzi wa amani ya Kimataifa.
Amesema pia kuwa, ni kwa kutambua wajibu huo ,ndiyo sababu iliyoifanya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kufikia makubaliano na nchi wanachama wenzie katika SADC na Maziwa Mkuu ( ICGLR), kujitolea kupeleka wanajeshi wake huko DRC ili kuunga mkono juhudi za kuwasaidia wananchi wa DRC kuwa na amani , usalama na maisha yenye uhakika.
Balozi Mwinyi amesema kuwa Tanzania inajivunia kuwa wanajeshi wake wanaohudumu kupitia FIB ambayo ni sehemu ya MONUSCO licha ya mazingira magumu na hatari wanayokabiliana nayo wameonyesha umahiri mkubwa ikiwa ni pamoja na kujitoa muhanga maisha yao kuwalinda raia wasiokuwa na hatia DRC pamoja na kurejesha amani na usalama.
0 comments:
Post a Comment