November 26, 2014

  • WARUNDI KORTINI KWA MENO 18 YA TEMBO


    WARUNDI KORTINI KWA MENO 18 YA TEMBO

    RAIA watatu wa Burundi akiwemo mwanamke wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi wa Wilaya ya Morogoro, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kuhujumu uchumi baada ya kukamatwa na meno ya tembo 18, na mikia mitano ya twiga, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 357.



    Watuhumiwa hao walipandishwa mahakamani jana na kusomewa mashitaka matatu na Wakili wa Serikali, Edgar Bantulaki, mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Alisile Mwankejela.
    Wakili huyo aliwataja watuhumiwa walioshitakiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukutwa na nyara ni John Lazaro Yantoro (55), Ibrahim Nena Yantoro (28) na Scolastica Aron (27), wote walikuwa wakiishi katika Kambi ya Wakimbizi ya Katumba Mpanda mkoani Katavi.
    Wakili huyo alidai watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 13, mwaka huu eneo la Bwawani mkoani Morogoro wakiwa na meno 18 ya tembo, yenye thamani ya dola za Marekani 135,000, sawa na Sh milioni 229.5.
    Pia, walikamatwa na nyara nyingine za mikia mitano ya twiga, ikiwa na thamani ya dola 75,000 sawa na Sh milioni 127.5. Alidai watuhumiwa hao walikuwa wakifanya biashara ya kununua na kuuza nyara hizo, zitokanazo na wanyama, mali ya Serikali.
    Alidai kutokana na kesi hiyo kuwa ni ya uhujumu uchumi, mahakama hiyo haina uwezo wa kuiendesha, isipokuwa kuwasomea mashitaka yao na wao kutotakiwa kujibu lolote. Upelelezi wa kesi hiyo unaendelea.
    Kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilishwa, Wakili wa Serikali aliiomba Mahakama kuipangia tarehe nyingine, ambapo hakimu wa mahakama hiyo aliiahirisha hadi Desemba 10 mwaka huu, itakapofikishwa tena mahakamani hapo kwa kutajwa.
    Aliamuru watuhumiwa hao kurudishwa rumande.

    HABARI LEO.

  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.