KATIKA kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, vijana 25 wamepatiwa mafunzo ya wasaidizi wa kisheria Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Msaada wa kisheria cha Mbeya Paralegal Unit(Mbepau), Jane Lawa, aliliambia gazeti hili kuwa kituo chake kimeona kutoa mafunzo kama hayo kutokana na kukithiri kwa matukio ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto na wanawake mkoani Mbeya.
Alisema mafunzo hayo yametolewa kwa vijana 25 kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya yaliyoanza Novemba 17 na kufungwa Novemba 21, Mwaka huu katika ukumbi wa Coffee Garden uliopo mjini hapa kwa ufadhili wa Legal Services Facility(LSF) mafunzo yaliyofundishwa na Mtaalamu kutoka Chuo kikuu Mzumbe.
Lawa alisema lengo la kutoa mafunzo kama hayo kwa vijana ni kupanua wigo wa kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa msaada wa kisheria kutoka ngazi ya kaya kwa kuwa vitendo vingi huwakumba watu maskini lakini wanashindwa kutoa taarifa kutokana na kutoelewa njia sahihi ya kupita na kupata msaada.
Aliongeza kuwa Jiji la Mbeya pekee linaKata 36 lakini vijana waliojitokeza ni kutoka Kata 25 tu jambo linalosababishwa na vijana kukataa kufanya kazi za kujitolea na kutanguliza maslahi mbele hivyo kupelekea idadi ndogo ya vijana kujitokeza katika mafunzo hayo.
Baadhi ya vijana waliopatiwa Mafunzo hayo walisema wamepata manufaa kutokana na kuongeza uelewa juu ya masuala ya kisheria na kuahidi kusaidiana na asasi zingine kupiga vita ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kwa kutoa elimu na misaada ya kisheria pindi itakapohitajika.
Mathias Halawa kutoka kata ya Mabatini na Halima Mbelwa kutoka Kata ya Forest walisema kupitia mafunzo hayo wataweza kuwasaidia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa kuwashauri njia za kupita ili waweze kupata haki zao kwa muda unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kwenye vyombo vya Sheria kama Polisi na Mahakamani.
Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo, Nuhu Suleiman kutoka Chuo kikuu Mzumbe Tawi la Mbeya, alisema ili kuboresha na kupanua huduma za msaada wa kisheria ni vizuri kujenga ushirikiano na taasisi zote zinazofanya kazi za namna hiyo kama Jeshi la Polisi na Mahakama pamoja na Wanasheia wa Serikali na Mawakili.
Alisema vijana hao amewafundisha Haki za binadamu, Ulinzi wa haki za binadamu hususani za Wanawake kama kundi maalumu, ukatili wa kijinsia na ujengwaji wa uwezo kisheria ili waeze kuongeza upana wa uelewa wa masuala ya kisheria kwa jamii wanazotoka.
Na Mbeya yetu
0 comments:
Post a Comment