February 25, 2016

  • Shule nne tu za serikali zapenya kati ya 100 bora kidato cha nne


    Shule nne tu za serikali zapenya kati ya 100 bora kidato cha nne

    Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba.

    Hali mbaya kwa shule za serikali imeendelea kujidhihirisha baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kutoa orodha ya shule zote zilizofanya Mtihani Novemba, mwaka jana na kuonyesha hakuna hata shule moja ya serikali kwenye 50 bora.
     
    Katika kundi la shule zenye watahiniwa zaidi ya 40, kati yake ndipo zilipo nne za serikali zilizofanikiwa kupenya 100 bora.
     
    Katika kundi hilo lenye shule 3,452 nchi nzima, shule za serikali zilizofanikiwa kuwa kwenye 100 bora ni Ilboru ya Arusha iliyokuwa ya 53, Kibaha ya Pwani iliyoshika nafasi ya 69, Mzumbe ya Morogoro ambayo ni ya 71 na Kilakala ya Morogoro iliyoshika nafasi ya 94.
     
    Shule ya kwanza kitaifa ni Kaizirege ya Kagera ikifuatiwa na Shule ya Wasichana ya Alliance (Mwanza), St. Francis (Mbeya), Shule ya Wavulana ya Alliance (Mwanza), Canossa (Dar es Salaam) na Shule ya Wavulana ya Marian (Pwani).
     
    Nyingine ni Alliance Rock Army (Mwanza), Shule ya Wasichana ya Feza (Dar es Salaam), Shule ya Wavulana ya Feza (Dar es Salaam) na Uru Seminary (Kilimanjaro).
     
    Shule nyingine ni Msolwa (Morogoro), Precious Blood (Arusha), Abbey (Mtwara), Shule ya Wasichana ya Marian (Pwani), Shule ya Wavulana ya Tengeru (Arusha), Rosmini ya Tanga, Shule ya Wasichana ya Josiah (Kagera), Katoke Seminari (Kagera), Don Bosco Seminary (Iringa) na St. James Seminari ya Kilimanjaro.
     
    Nyingine ni Loreto ya Mwanza, Kifungilo (Tanga), St. Joseph's Iterambogo Seminari (Kigoma), St. Mary's Mazinde Juu (Tanga), St. Amedeus (Kilimanjaro), Boniconsili Mabamba (Kigoma), Barbro-Johansson (Dar es Salaam), Morning Star (Mwanza), Scolastica ya Kilimanjaro na Kasita Seminari ya Morogoro.
     
    Katika kundi hili pia kuna Shule ya Nyegezi Seminari (Mwanza), Kanyigo ya Kagera, Joyland ya Kilimanjaro, Pandahill (Mbeya), St. Mary's-Ulete (Iringa), Uwata (Mbeya), Holy Family (Mwanza), Queen of family (Shinyanga), Itaga Seminari (Tabora), St. Marie Eugenie (Kilimanjaro) na Shule ya Wasichana ya Peramiho ya Ruvuma.
     
    Shule ya Olympus ya Mara, Shule ya Wasichana ya St. Clare Biharamulo (Kagera), St. Ann's Seminari (Morogoro), St. Clara (Kilimanjaro), St. Luise Mbinga (Ruvuma), Anderlek Ridges (Shinyanga), Kandoto Sayansi (Kilimanjaro), Shule ya Wasichana  Premier (Pwani) na Mivumoni Islamic Seminari ya Dar es Salaam ni shule zilizo kwenye Kundi la 50 bora.
     
    Nyingine zilizo kwenye Kundi la100 bora ni Henry Gogarty ya Arusha, Star (Arusha), Ilboru (Arusha), Carmel (Morogoro), Amani (Singida), St. Peter Claver (Dodoma), Genda (Manyara), Shule ya Wasichana ya Mother Teresa of Calcuta (Kilimanjaro), Huruma (Dodoma), Alpha (Dar es Salaam) na Palloti (Singida).
     
    Shule nyingine ni St. Joseph Millenium (Dar es Salaam), St. Francis de Sales Mission (Tabora), Kowak (Mara), Maua Seminari (Kilimanjaro), Famgi (Mwanza), Makoko Seminari (Mara), Lake (Mwanza), Kibaha (Pwani), St. Joseph Seminary ya (Mwanza), Mzumbe (Morogoro), Charlotte (Morogoro), St. Getrude Mlandizi (Pwani), Maria de Mattias (Dodoma) na Geita Adventist ya Geita.
     
    Nyingineni ni Sekondari ya Kitungwa ya Morogoro, St. Peter's Seminari (Morogoro), St. Mary Goreti (Kilimanjaro), Bendel Memorial (Kilimanjaro), Sanu Seminari (Manyara) na Shule ya Wasichana ya Visitation (Kilimanjaro).
     
    Sekondari nyingine ni Murutunguru (Mwanza), St. Rufino and Ronaldo Agr (Kigoma), Stanley (Dar es Salaam), Loyola (Dar es Salaam), Tusiime (Dar es Salaam), Oswe (Mbeya), Kidugala Lutheran Seminar (Njombe), Mbezi Beach (Dar es Salaam), Ritaliza (Kilimanjaro) na Shule ya Wavulana ya St. Stephen (Kilimanjaro).
     
    Nyingine zilizo kwenye kundi hili ni ile ya Wasichana ya Kibosho ya Kilimanjaro, Agape Lutheran Seminari (Kilimanjaro), Kilakala (Morogoro), Shule ya Wasichana ya St. Francis of Assisi (Dodoma), Masama (Kilimanjaro), St. Francis Xavier (Kigoma), Stella Matutina Lighano Seminari (Ruvuma), Shule ya Wavulana ya Living Stone Seminari (Tanga) na Trust Patrick (Arusha).
     
    Katika mtihani huo ambao shule nyingi za mwisho ni zile za serikali, watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 9,816 sawa na asilimia 2.77, daraja la pili 31,986 sawa na asilimia 9.01, daraja la tatu 48,127 sawa na asilimia 13.56, daraja la nne 151,067 sawa na asilimia 42.57 na wale wa sifuri ni 113,489 sawa na asilimia 32.09.
     
    MAONI YA WADAU
    Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, akitoa maoni yake kuhusiana na shule za sekondari za serikali kuendelea kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa, alisema sababu kubwa ni mazingira mabaya.
     
    Mukoba alisema kinacholeta matokeo mabaya katika shule hizo ni mazingira ya shule  kuharibika huku kukiwa hakuna huduma muhimu kama chakula, vitanda na maji.
     
    "Kama mazingira ni mabovu vipaji vya wanafunzi hao vinazalishwaje?," alihoji Rais huyo wa CWT na kuongeza:
     
    "Walimu nao wamekata tamaa, wanaona wabunge wanapewa magari wao hakuna, kazi yao ni kutoa vipaji tu nao wameona huo ni wendawazimu."
     
    Alisema ili kunusuru elimu katika shule hizo, lazima serikali iboreshe mazingira kwa kuhakikisha huduma zote zinapatikana.
     
    Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten Met), Cathreen Sekwao, alisema sababu kubwa ya kushuka kwa elimu kwenye shule hizo ni huduma maalum zilizopaswa kuwapo zimelegalega ikilinganishwa na hapo awali.
     
    "Hakuna vitabu vya kutosha, hakuna walimu wazuri, mazingira yenyewe siyo rafiki shule hazifanyiwi ukarabati, kwa ujumla hali siyo nzuri katika shule hizi, zitawezaje leo kuitwa za vipaji maalum?," alisema na kuongeza:
     
    "Tumekuwa tukiziangalia shule mpya za kata, hizi zimesahaulika hata matengenezo hazifanyiwi tena, zimechoka." 
     
    Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Taasisi Binafsi za Elimu Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya, alisema kufanya vibaya kwa shule hizo ni suala la kisera ambalo limewafanya wanafunzi kubweteka badala ya kusoma.
     
    "Tumeshuhudia matokeo haya yameonyesha wazi kuwa mfumo wa zamani wa divisheni umewaangusha wengi ule uliokuwa ukitumika ulikuwa unawabeba," alisema.
     
    Pia alisema serikali inatakiwa kuona uwezekano wa kutumia mfumo wa 'vocha' ambao umefanikisha shule nyingi duniani ikiwamo Uganda ambayo mzazi anachukua ada serikalini na kuchagua mwenyewe shule anayotaka.
     
    Alisema utaratibu huo umepandisha hadhi za shule na kupunguza gharama na kuwafanya wenye shule kushindana kuboresha shule zao ili wazazi wazichague.
     
    "Huu ni utaratibu mzuri badala ya serikali kumchagulia mtoto shule, mzazi anachagua mwenyewe," alisema.
    CHANZO: NIPASHE


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.