February 27, 2016

  • Tanzania kunufaika na Dola Bilioni 60 za China sekta ya Nishati


    Tanzania kunufaika na Dola Bilioni 60 za China sekta ya Nishati
    Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam,

    Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeitaja nchi ya Tanzania kuwa na nafasi kubwa ya kunufaika na fedha kiasi cha Dola Bilioni 60 kupitia uwekezaji sekta ya nishati, fedha zilizoahidiwa kutolewa na nchi hiyo wakati wa Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Ushirikiano baina ya China na Afrika, uliofanyika nchini Afrika Kusini mwezi Desemba,2015.

    Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa China nchini, Dkt. Lu Youqing na ujumbe wake alipokutana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa, China ina imani kubwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyosimamia masuala mbalimbali nchini, pia Profesa Sospeter Muhongo kutokana na namna anavyoisimamia sekta ya Nishati na Madini.

    Miongoni mwa Sekta zinazopewa kipaumbele katika fedha hizo ni pamoja na pamoja na miundombinu, afya, biashara, uwekezaji na kupunguza umaskini, barani Afrika.

    Kutokana na mahusiano mazuri ambayo yamekuwepo kwa miongo kadhaa baina ya nchi hizo mbili, Balozi Youqing amemwakikishia Waziri Muhongo kuwa, China itaendeleza ushirikiano huo kwa kuhakikisha inazishawishi kampuni kubwa na zilizobobea kitaalamu na kiteknolojia za China, ili ziweze kushirikiana na Tanzania katika sekta ya nishati, na zaidi katika uzalishaji umeme kwa kutumia Makaa ya Mawe kutokana na namna ambavyo Wizara inavyokipa kipaumbele chanzo hicho kuzalisha umeme nchini.

    Wakati huo huo, China imesema itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi Watanzania kusoma masuala ya mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali nchini humo kutokana na umuhimu wa sekta hiyo na kwamba, China inapenda Tanzania ifanikiwe katika kuzalisha wataalam wa kutosha katika fani hizo na kuongeza kuwa, anatambua juhudi zinazofanywa na Waziri Muhongo kuhakikisha wanafunzi wengi wa kitanzania wanapata fursa ya kusoma masuala ya mafuta na gesi maeneo mbalimbali Duniani, ikiwemo China.

    Aidha, leo tarehe 26 Februari, 2016, Wizara ya Nishati imetangaza nafasi za Masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kuomba kusoma katika Vyuo vya China katika fani za Mafuta na Kazi katika ngazi za Shahada ya Uzamili (Masters) na Uzamivu (Phd). Maelezo zaidi ya kuomba nafasi hizo yanapatikana kupitia tovuti ya wizara www.mem.go.tz
    Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akiongea jambo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China, Dkt. Lu Youqing (wa pili kushoto) wakati alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Afisa Ubalozi wa China.
    Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Dkt. Lu Youqing (wa tatu kushoto), akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Utumishi Wizara ya Nishati na Madini, Lusias Mwenda. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Balozi wa China.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.