Tunakujali, Tunakuthamini na Pia Tunakupenda!

February 27, 2016

  • VURUGU ZA MACHINGA ZAZUWA TAFRANI JIJINI MBEYA....


    Baadhi ya Vibanda vya Biashara vya Wafanyabiashara Ndogondogo Maarufu kama Machinga Vikiteketea kwa Moto mara baada ya Wafanya Biashara hao wa Eneo la Sido na Stendi ya Kabwe Jijini Mbeya kuanzisha Vurugu Baada ya Kubomolewa Vibanda vyao vya Biashara katika maeneo waliyokuwa wakifanyia Biashara Zao.
    Jitihada za kuzima Moto ulio washwa na Wamachinga wa Kabwe na Sido zikifanyika kutoka kwa Jeshi la Zima Moto Jiji la Mbeya katika Vurugu zilizo Dumu kwa Muda kuanzia Asubuhi ya Leo na kupelekea Wamachinga hao Kuchoma Matairi Barabarani na Baadhi ya Masalia ya Vibanda vyao mara baada ya Kubomolewa Vibanda vyao vya Biashara.
    Jeshi la Polisi kikosi cha kutuliza Ghasia kikiwa Ngangari kuhakikisha hali ya Usalama ina kuwa Shwari na Vurugu kutoendelea...
    Baadhi ya wapiga Debe wa Stendi ya Kabwe wakiwa hawana nongwa na Mtu bali wakiendelea kutimiza agizo la Rais Dkt.John Pombe Magufuli kufanya Usafi kila Juma Mosi ya mwisho wa Mwezi na hapo wakiwa Sambamba na Vifaa vyao vya kufanyia Usafi mbele ya Jeshi la Polisi kama waonekanavyo katika Taswira.
    PICHA ZOTE NA MR.PENGO MMG MBEYA.

  • BENKI YA NMB MBEYA YAZINDUA KITUO CHA BIASHARA (NMB BUSINESS CENTER)


    BENKI YA NMB MBEYA YAZINDUA KITUO CHA BIASHARA (NMB BUSINESS CENTER)
    Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa NMB Business Center Mkoa wa Mbeya akizungumza na wafanyabiashara katika uzinduzi huo
    Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi Ineke Bussemaker akiwakaribisha wafanyabiashara waliofika katika uzinduzi wa NMB Business Center Jijini Mbeya
    Mkuu wa Idara ya Biashara Bw. James Meitaron akimfafanulia jambo Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi. Ineke Bussemaker. Anaeshuhudia katikati ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi wa benki hiyo Bw. Abdulmajid Nsekela.
    Mgeni rasmi katika uzinduzi wa kituo cha biashara cha NMB (NMB BUSINESS CENTER) Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi. Ineke Bussemaker na Afisa Mkuu wa Huduma kwa Wateja Binafsi Bw. Abdulmajid Nsekela katika uzinduzi wa kituo hicho hivi karibuni.
    Meneja wa NMB Business Center Jijini Mbeya Bi. Mary Ngalawa akimuonyesha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bi. Ineke Bussemaker maeneo mbalimbali ya kituo hicho.
    Benki ya NMB imezindua kituo cha biashara (NMB BUSSINESS CENTER) mkoani Mbeya kitakachokuwa kikihudumia wateja wafanyabiashara na kuboresha uendeshaji wa biashara kwa wateja wafanyabiashara katika Mkoa huo.
    Akiongea katika uzinduzi wa kituo hicho Afisa Mkuu wa wateja binafsi wa NMB Abdulmajid Nsekela amesema kuwa lengo la vituo vya biashara kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini ni kuboresha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na hivyo kuchangia katika kuchochea ufanisi wa wafanyabiashara na kukuza uchumi. Hivyo wanataraji kuendelea kuwafikia wafanyabiashara popote walipo kwa huduma bora.
    Aidha Afisa huyo wa Wateja Binafsi ameeleza kuwa katika mpango huo wanataraji kufanikisha malengo ya wateja wao ambao ni wafanyabiashara wakubwa, wa kati, wadogo sambamba na wakulima kwa kuboresha biashara ya kilimo.
    Pia Bw. Nsekela amefahamisha kuwa pamoja na kufanya shughuli za kibenki, NMB pia inachangia shughuli za kijamii katika kuchangia maendeleo na wanatenga pato lao la mwaka kama mchango wao katika sekta ya afya na elimu ikiwa na lengo la kuiunga mkono Serikali ambapo wanatenga asilimia moja katika pato la mwaka kufanya shughuli hizo. 
    Afisa huyo wa NMB amewataka wateja wa kati kuchangamkia fursa hiyo ambayo inawapa nafasi wafanyabiashara kupanda kutoka daraja moja kwenda lingine kulingana na ufanisi wa vituo vya biashara na elimu ya kifedha watakayopatiwa na NMB. 
    Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi wa kituo cha biashara cha NMB mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro amewataka wafanyabiasha na wakazi wa Mkoa huo kutumia fursa za kibenki ambazo zinatolewa ili kufikia malengo yao ya kibiashara.
    Mh. Kandoro amefahamisha kuwa kabla ya kuchukua mkopo wanatakiwa kufanya tathmini na kujua biashara gani wanaweza kufanya na kuweza kufanya marejesho ya benki.
    Pia Mh. Kandoro aliwataka viongozi wa benki ya NMB kuangalia suala la riba katika mikopo wanayotoa kwa vile wananchi wengi wanaogopa kukopa kutokana na baadhi ya mabenki nchini kutoza riba kubwa jambo linalowawia vigumu wafanyabiasha wadogo kujenga kasumba ya kuhofia mikopo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi na kupanua wigo wa biashara zao. 
    Benki ya NMB pia imejikita kwenye shughuli za kilimo kwa kuwezesha urahisi wa upatikanaji wa pembejeo ambapo hivi karibuni wameanzisha mpango wa kuwapatia wateja wake matrekta kwa gharama nafuu baada ya kuingia mkataba na kampuni ya Jebiz ambao ni wasambazaji wa matrekta.
    Benki ya NMB ina matawi 175, Mashin za kutoa pesa (ATM) zaidi ya 600 na Mawakala ambao wanarahisisha shughuli za kibenki zaidi ya 450 pia wamejiunga na mitandao ya simu yanayotoa huduma za kifedha kwa njia ya simu. 
    Kwa upande wa mikopo Mkuu wa Kitengo cha Biashara Bw. James Meitaron ameeleza utaratibu mzima wa utoaji wa mikopo kwamba kiwango ambacho wanaanzia kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ni kuanzia Shilingi milioni moja hadi milioni thelathini (milioni 30) mkopo ambao unapatikana ndani ya siku mbili na kuwa benki hiyo imempa mamlaka Meneja wa tawi kufanikisha mikopo ya kiwango hicho.
    Kama biashara yako imeanza kukua, kituo cha biashara ambapo kwa Mbeya kipo NMB Mwanjelwa kinatoa mkopo kuanzia milioni 30 hadi bilioni 2.
    Meitaron amesema kuwa riba ya mikopo kwa benki hiyo haizidi asilimia 23 kwa mwaka na kadiri unavyolipa mkopo riba inapungua mpaka kufikia asilimia 18 kulingana na mkopo uliokopa.


  • TANESCO Yapeleka Maombi ya Kupandisha Bei Ya Umeme


    TANESCO Yapeleka Maombi ya Kupandisha Bei Ya Umeme

    SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limepeleka maombi kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuomba kupandisha bei ya nishati hiyo, kinyume na matakwa ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ya kushusha bei hiyo.
     
    Taarifa ya Ewura kwa umma iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana, imeeleza kuwa maombi hayo yamepokewa Jumatano ya wiki hii na kutaka wadau kujitokeza kujadili uhalali wa nyongeza hiyo siku mkutano huo utakapoitishwa.
     
    "Mamlaka inaanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau, ili kujua uhalali wa maombi ya nyongeza ya bei za huduma iliyoyapokea kutoka Tanesco," imeeleza taarifa hiyo.
     
    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanesco iliwasilisha ombi husika kulingana na Sheria ya Umeme namba 131, inayoitaka Ewura kufanya mabadiliko ya bei zinazotozwa na mtoa huduma mara moja kila baada ya miaka mitatu.
     
    "Pendekezo la wastani wa badiliko la bei za umeme ni asilimia 1.1 kuanzia Aprili mosi 2016 na asilimia 7.9 kuanzia Januari mosi 2017,"limeeleza tangazo hilo.
     
    Mapendekezo hayo japo ya kisheria, lakini yanapingana na msimamo wa Waziri Muhongo, ambaye tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, alielezea kusudio lake la kutaka bei ya nishati hiyo ishushwe.
     
    Profesa Muhongo alikwenda mbali na kuagiza Tanesco, Ewura na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa bei ya umeme kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.
     
    Katika maagizo hayo, Profesa Muhongo alihoji kwa nini bei ya umeme isishuke, wakati gharama za uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta zimeshuka kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
     
    Kutokana na maombi hayo ya Tanesco, Ewura imewataka wadau wa nishati wanaopenda kutoa maoni yao kwa maandishi, kufanya hivyo kwa kutuma maoni yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, ghorofa ya saba jengo la LAPF Pensions Fund Tower, mkabala na Kijiji cha Makumbusho, Kijitonyama Dar es Salaam.
     
    Kwa watakaotuma kwa njia ya posta, wameombwa kufanya hivyo kwa kutumia Sanduku la Posta 72175, Dar es Salaam, Tanzania, simu namba (+255-22) 2123853-4; Fax namba (+255-22) 2123180; Barua pepe info@energyregulators.org au tovuti http://www. energyregulators. org.
     
    Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamlaka hiyo pia, itaitisha mikutano ya wazi ili kukusanya maoni kuhusu mapendekezo hayo kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwamo Baraza la Wawakilishi wa Watumiaji wa Huduma (CCC); Baraza la Ushauri la Serikali (GCC) pamoja na wananchi kwa ujumla.


  • Adhabu saba kwa mawaziri 5 waliokaidi agizo la maadili



    Adhabu saba kwa mawaziri 5 waliokaidi agizo la maadili
    Pamoja na mawaziri wa tano wa Rais John Magufuli kuwasilisha fomu za tamko la rasilimali na madeni na kiapo cha uadilifu kukwepa kihunzi cha kutumbuliwa majipu na bosi wao, vigogo hao wanabanwa na adhabu saba kwa kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, ikiwamo kushushwa cheo au kusimamishwa kazi.
    Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwaambia wanahabari jijini hapa jana kuwa viongozi wa umma wanaoshindwa kuwasilisha fomu hizo ndani ya siku 30 zinazotakiwa kisheria, hutakiwa kutoa maelezo na iwapo hayataridhisha mamlaka husika huchukua hatua za kinidhamu.

    Kifungu 9(1)(b) cha sheria hiyo kinawataka viongozi wa umma kuwasilisha matamko yao ndani ya siku 30.

    Majaliwa aliwataja mawaziri waliozidisha muda huo na kushindwa kuwasilisha fomu hizo kwa wakati kuwa ni January Makamba ambaye ni Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Charles Kitwanga (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) na Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

    Mawaziri wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina.

    Alisema kutokana na kutotimiza masharti hayo, Rais Magufuli aliwaagiza mawaziri hao kuzipeleka fomu hizo mapema iwezakanavyo kabla ya saa 12 jioni jana, la sivyo wangekuwa wamejiondoa wenyewe kwenye madaraka waliyonayo.

    Mawaziri hao jana mchana ama wao au kwa kuwatuma wawakilishi, waliwasilisha fomu hizo hivyo kukwepa adhabu ya awali iliyokuwa imetolewa na Rais ya kujiondoa wenyewe kwenye mamlaka waliyonayo.

    Hata pamoja na kuruka adhabu hiyo ya awali, bado sheria hiyo ya maadili inatoa moja ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kwa viongozi wa umma iwapo watakiuka masharti ya sehemu ya tatu inayojumuisha kifungu cha 9 (1)(b), zilizobainishwa katika kifungu cha nane.

    "Masharti katika sehemu hii yatakuwa ni sehemu ya maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ukiukwaji wa maadili utasababisha kuchukuliwa hatua mojawapo, yaani (a) kuonywa na kupewa tahadhari; (b) kushushwa cheo na (c) kusimamishwa kazi," kinaeleza kifungu cha sheria hiyo iliyojumuisha mabadiliko ya mwaka 2002 na kuongeza hatua nyingine ambazo ni:
    "(d) kufukuzwa kazi; (e) kumshauri kiongozi kujiuzulu wadhifa unaohusu ukiukaji huo; (f) kupewa adhabu nyingine zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nidhamu kuhusu wadhifa wa kiongozi na (g) kuhimiza kuchukuliwa hatua kwa kiongozi kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo."

    Hadi jana wakati Waziri Mkuu anatoa agizo hilo la Rais la kuwataka kuwasilisha fomu hizo haraka kabla hawajatumbuliwa majipu, Makamba, Mpina, Kitwanga na Balozi Mahiga walikuwa wameshatimiza siku 46, baada ya muda wa mwisho wa kurudisha fomu hizo kisheria kukamilika.

    Profesa Ndalichako alikuwa ametimiza siku 63 tangu ateuliwe hivyo alikuwa ameshapitisha siku 33 baada ya muda rasmi unaotakiwa kisheria kuwasilisha fomu hizo kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma.

    "Mheshimiwa Rais ameelekeza majina yao yasomwe ili popote walipo warudi na watekeleze agizo hilo na ofisi yangu itasimamia kikamilifu kuhakikisha fomu hizo zinawasilishwa kama inavyotakiwa," alisema Majaliwa.

    Kamishna wa Sekretarieti wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome Kaganda ambaye juzi aliwasilisha majina ya mawaziri hao kwa Majaliwa, alisema vigogo wote hao walizishawasilisha fomu hizo.

    Mawaziri wawasilisha fomu
    Baada ya agizo la Rais Magufuli kutolewa na Waziri Mkuu jana saa sita mchana hadi saa 9.30 alasiri mawaziri wanne na naibu waziri mmoja walikuwa wamewasilisha fomu zao na kumpa nafasi Jaji Kaganda kuondoka ofisini kwake saa 10 jioni.

    Mawaziri Dk Mahiga, Kitwanga na Mpina walifika wenyewe kwenye ofisi hiyo na kukabidhi fomu zao, wakati Profesa Ndalichako na January walituma wawakilishi wao kupeleka fomu hiyo.
    Makamba alisema jana kuwa alishawasilisha fomu hizo tangu saa 8:00 mchana na kueleza kuwa zilikuwa zimejazwa tangu mkutano wa kwanza wa Bunge la 11, Novemba mwaka jana.

    "Miaka yote huwa namtumia mwanasheria wangu wa siku nyingi ambaye huwa anazihakiki fomu na kugonga muhuri wa kiapo na kuziwashilisha Sekretarieti, lakini kwa bahati mbaya safari hii alipata hudhuru wa muda mrefu na mtu niliyemtuma hakunieleza jambo hilo.

    "Siku zote nilikuwa naamini kuwa zimeenda na sikuwa na wasiwasi wa kwenda kufuatilia, lakini nilivyosikia kuwa hazijafika ilibidi tukazichukue nizijaze haraka na kuziwasilisha haraka hata kabla ya kunifikia barua rasmi," alisema Makamba.

    Mpina aliyekuwa wa mwisho kuwasilisha fomu hizo alisema alikuwa na sababu ya kuchelewa kujaza , lakini kwa hali ilivyo inaonyesha kuwa Rais hakukubaliana nazo hivyo kutoa agizo ambalo amelitii baada ya kufanikiwa kupata taarifa zilizomzuia kukamilisha.

    "Binafsi sina malalamiko na hilo agizo ndiyo maana nimejaza, ila kilichonichelewesha sikuwa na taarifa za mshahara wangu, lakini baada ya agizo la Rais kuna mawasiliano yalifanyika mhasibu alikuja leo ofisini kwangu tukajaza wote ndiyo nimezileta hapa," alisema Mpina.
    Alisema kuwa: "Ukiona hivyo kwamba bwana mkubwa (Rais Magufuli) ametoa saa 12 ina maana sababu zetu zimekataliwa, maana jana (juzi) kwenye kikao tulikubaliana kwamba mwisho iwe mwezi wa nne, lakini nafikiri alilikataa hilo."

    Dk Mahiga alisema kuwa alipeleka fomu hizo kabla ya saa 6:00 mchana baada ya kushindwa kuziwasilisha mapema kisheria kutokana ratiba ngumu ya kazi aliyonayo.
    "Natumia muda mwingi kusafiri na kuhudhuria mikutano kama wadhifa wangu unavyonitaka, hata mheshimiwa Rais anafahamu hili nilishamueleza.

    "Kiufupi tangu nianze kazi, nimetumia nusu ya muda wangu kwenda nje ya nchi kuliko hapa nyumbani, lakini agizo la jana lilikuwa ni ukumbusho mwema," alisema Mahiga huku akibainisha kuwa amekuwa akijaza fomu hizo kwa miaka zaidi ya 40 bila kumletea matatizo.

    Hata wakati Balozi Mahiga akieleza hayo, Waziri Kitwanga aliilaumu Sekretarieti kuwa alikuwa ameziwasilisha fomu hizo tangu Januari 4, lakini zilikuwa hazionekani baada ya ufuatiliaji jana zilipatikana. "Nilikutana na Kamishna (Jaji Kaganda) na alinieleza kuwa wameshazipata fomu hizo," alisema.

    Jana jioni taarifa kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema kuwa agizo hilo la Rais Magufuli la kuwataka mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni wakamilishe kabla ya saa 12 lilitekezwa ipasavyo.

    "Waziri Mkuu amepokea barua kutoka kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome Kaganda ikithibitisha kuwa mawaziri na naibu mawaziri wote wametekeleza agizo hilo.

    "Hadi kufikia saa 9.30 leo(jana) alasiri mawaziri wote walikuwa wamekamilisha fomu zao za kuzikabidhi katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma," alisema Waziri Mkuu.
    Wakati huo huo; Majaliwa alisema Serikali itaendelea na mtindo wake wa kuwawajibisha viongozi wasio waadilifu na kuwataka watendaji wote waliopewa ridhaa ya uongozi kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu mkubwa.

    Alisema hayo jana jioni alipozungumza na viongozi wa dini, akifafanua kuwa Serikali haitamuonea yeyote na itatenda haki kwa kila mmoja. Alikuwa akijibu hoja ya Askofu wa Anglikana, Valentino Mokiwa aliyesema utumbuaji majipu unapunguza kasi ya utendaji na kuwajengea hofu watumishi.


  • Watorosha makontena wasalimisha mali za Bn 6/-


    Watorosha makontena wasalimisha mali za Bn 6/-

    Kampuni ya udalali ya Yono, imesema makampuni na wafanyabiashara wanaodaiwa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kutorosha makontena kwenye Bandari Kavu ya Azam mwaka jana, wamekabidhi mali  zinazokadiriwa kufikia Sh. Bn 6.
     
    Mali hizo zitauzwa ili kulipa kwa TRA fidia ya kodi ya jumla ya Sh. bilioni 18 ambazo zilikwepwa kulipwa na wafanyabiashara na kampuni hizo.
     
    Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa kampuni ya udalali ya Yonno iliyopewa kazi ya kuzifilisi kampuni zilizokwepa kodi, Stanley Kevela, alisema wafanyabiashara wengi wameonyesha ushirikiano wa kulipa deni hilo la serikali.
     
    "Tulitaka kuanza kufunga maduka na mali za wahusika lakini katika hali ambayo hatukuitarajia wengi wanatoa ushirikiano mzuri na Kampuni ya Yono na wengine wameendelea kutuambia kuwa watalipa madeni yao ndani ya muda mfupi," alisema Kevela.
    "Lengo letu siyo kuwatisha wafanyabiashara bali kuwezesha deni la serikali lilipwe."
     
    Mwenyekiti huyo wa Yono alisema hadi sasa wafanyabiashara mbalimbali wameshasalimisha kwa TRA zaidi ya Sh. milioni 300, baada ya kupewa hesabu za madeni wanayodaiwa.
     
    Kevela alisema wameanza kamatakamata ya mali za wafanyabiashara wanaodaiwa na mamlaka hiyo lakini wale wanaoonyesha ushirikiano mzuri hawafungi wala kuchukua mali zao kwani huelewana namna bora ya kulipa.
     
    "Kote tunakoenda kwa ajili ya kukamata mali imetushangaza kuona hakuna anayekataa kulipa hilo deni, wote wamesema watalilipa na wengine wanataka kupewa muda kidogo ili wajipange jambo ambalo ni zuri," alisema Kevela.
     
    "Sisi tutashirikiana nao kuhakikisha fedha za serikali zinapatikana."
     
    Alisema mali zinazofikia Sh. bilioni sita ambazo wafanyabiashara wameikabidhi Yono zitauzwa kwa mnada ili zipatikane fedha za kwenda kulipa madeni ya wafanyabiashara hao kwa TRA.
     
    "Sisi hatutaki kufanya kazi hii kwa kukurupuka na kwa jazba, tunakwenda kisomi na kwa mbinu za kisasa maana tunataka kuwaelimisha zaidi wafanyabiashara badala ya kutumia nguvu na kwa kweli mbinu hii inatusaidia kupata ushirikiano mkubwa.
     
    "Kuna mfanyabiashara anadaiwa Sh. bilioni saba... tulitaka kukamata mali zake lakini kaonyesha ushirikiano kwamba atalipa hivi karibuni." 
     
    Yono ilishinda zabuni ya kuwa dalali wa TRA na wiki mbili zilizopita iliwapa siku 14 wafanyabiashara hao wawe wamelipa fedha wanazodaiwa na Mamlaka hiyo vinginevyo watafilisiwa.

    CHANZO: NIPASHE


  • WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA BALOZI WA KUWAIT NCHINI


    WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA BALOZI WA KUWAIT NCHINI
    Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. January Makamba (kushoto) akiongea na Balozi wa Kuwait Bw. Jasem Al-Najem, Balozi huyo alimtembelea Mh. Makamba Ofisini kwake leo Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadiliana masuala ya hifadhi na usimamizi wa Mazingira.
    Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. January Makamba (kushoto) akiongea na Balozi wa Kuwait Bw. Jasem Al-Najem, Balozi huyo alimtembelea Mh. Makamba Ofisini kwake leo Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadiliana masuala ya hifadhi na usimamizi wa Mazingira. Wengine katika picha ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makumu wa Rais Bw. Mbarak Abdulwakil na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje Bw. Barthlomew Jungu.


  • Tanzania kunufaika na Dola Bilioni 60 za China sekta ya Nishati


    Tanzania kunufaika na Dola Bilioni 60 za China sekta ya Nishati
    Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam,

    Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeitaja nchi ya Tanzania kuwa na nafasi kubwa ya kunufaika na fedha kiasi cha Dola Bilioni 60 kupitia uwekezaji sekta ya nishati, fedha zilizoahidiwa kutolewa na nchi hiyo wakati wa Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Ushirikiano baina ya China na Afrika, uliofanyika nchini Afrika Kusini mwezi Desemba,2015.

    Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa China nchini, Dkt. Lu Youqing na ujumbe wake alipokutana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa, China ina imani kubwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyosimamia masuala mbalimbali nchini, pia Profesa Sospeter Muhongo kutokana na namna anavyoisimamia sekta ya Nishati na Madini.

    Miongoni mwa Sekta zinazopewa kipaumbele katika fedha hizo ni pamoja na pamoja na miundombinu, afya, biashara, uwekezaji na kupunguza umaskini, barani Afrika.

    Kutokana na mahusiano mazuri ambayo yamekuwepo kwa miongo kadhaa baina ya nchi hizo mbili, Balozi Youqing amemwakikishia Waziri Muhongo kuwa, China itaendeleza ushirikiano huo kwa kuhakikisha inazishawishi kampuni kubwa na zilizobobea kitaalamu na kiteknolojia za China, ili ziweze kushirikiana na Tanzania katika sekta ya nishati, na zaidi katika uzalishaji umeme kwa kutumia Makaa ya Mawe kutokana na namna ambavyo Wizara inavyokipa kipaumbele chanzo hicho kuzalisha umeme nchini.

    Wakati huo huo, China imesema itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi Watanzania kusoma masuala ya mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali nchini humo kutokana na umuhimu wa sekta hiyo na kwamba, China inapenda Tanzania ifanikiwe katika kuzalisha wataalam wa kutosha katika fani hizo na kuongeza kuwa, anatambua juhudi zinazofanywa na Waziri Muhongo kuhakikisha wanafunzi wengi wa kitanzania wanapata fursa ya kusoma masuala ya mafuta na gesi maeneo mbalimbali Duniani, ikiwemo China.

    Aidha, leo tarehe 26 Februari, 2016, Wizara ya Nishati imetangaza nafasi za Masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kuomba kusoma katika Vyuo vya China katika fani za Mafuta na Kazi katika ngazi za Shahada ya Uzamili (Masters) na Uzamivu (Phd). Maelezo zaidi ya kuomba nafasi hizo yanapatikana kupitia tovuti ya wizara www.mem.go.tz
    Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akiongea jambo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China, Dkt. Lu Youqing (wa pili kushoto) wakati alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Afisa Ubalozi wa China.
    Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Dkt. Lu Youqing (wa tatu kushoto), akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Utumishi Wizara ya Nishati na Madini, Lusias Mwenda. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Balozi wa China.


  • Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.