Mjumbe wa kamati ya kuchunguza vikwazo visivyo vya kiforodha, Jimmy Mwalugelo (katikati) akizungumza. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Real Insurance, Stephen Okundi na kushoto ni SACP Kaimu Kamanda wa Trafiki nchini SACP Johansen Kahatano.
Mwalugelo akionesha vibao vitakavyoweka katika magari yaendayo nje ya nchi.
KAMATI ya kitaifa inayofuatilia vikwazo vya kibiashara visivyokuwa vya kiforodha na kuwakilisha sekta binafsi kupitia TAFFA, imetoa tamko kuhusu hatua itakazochukua kuwasaidia wafanyabiashara hasa wasafirishaji wa mizigo ya kibiashara pamoja na watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam na Maziwa Makuu waliopo nchini.
Akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam, mjumbe wa kamati hiyo, Jimmy Mwalugelo, alisema anaishukuru serikali na wafadhili kama vile Trade Mark East Afrika, USAID, JICA na wengine ambao wanawawezesha wafanyabiashara kufanya kazi zao bila usumbufu usio wa lazima.
Alisema kuwa kamati hiyo ina mipango ya kuanzisha kamati katika mipaka na idara zote za serikali na sekta binafsi (Joint Border Committees) ambazo hupaswa kukaa kila mwezi japo mara moja na kutatua kero zinazojitokeza za mpakani ili kuepusha ukwepaji wa kodi.
Alifafanua kuwa anaishukuru pia serikali kwa kukubali ombi lao la kuwa na ofisi za 'Clearing Agent' pamoja na JBC kwa ajili ya kuwapatia ofisi kwenye majengo ya pamoja yanayojengwa kwenye mipakani (One Stop Border Post) na USAID kwa kuwawezesha kuwapatia vitendea kazi kupitia TAN TRADE ambapo wametoa kompyuta, mashine za 'photocopy' na 'printer'.
Vilevile alisema kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi mpaka wa Tanzania na Rwanda huko Rusumo na upande wa Burundi katika mji wa Kabanga kulikuwa na vizuizi 58 lakini kwa juhudi zao wamefanikiwa kuvipunguza hadi kufikia sita na bado wanaendelea kufanya jitihada kuvipunguza zaidi.
Kamati hiyo ilifafanua kuwa imeweza kugundua matatizo yanayowapata madereva wanaoendesha magari yanayoenda nchi jirani pale wanapopata ajali njiani na wengine kupoteza maisha wakati magari hayajafika yanakokwenda.
"Matatizo yanayojitokeza ni kutojua gari lilikuwa linaenda nchi gani kutokana na kukosa alama ya kuonyesha nchi linakokwenda hivyo baadhi ya waagizaji wa magari hayo wanashindwa kuja mahali ilipotokea ajali na mahali lilipo gari," alisema.
Aidha alisema kamati imejielekeza katika sekta binafsi ambapo inahimiza kuwakatia bima (Real Insurance) madereva wanaoendesha magari yanayoenda nchi za jirani kwa kuwalipa mafao kidogo kwa ajili ya gharama za usafiri na kujikimu kwa matibabu wapatapo ajali njiani kwa mfano mtu akifariki ambapo hulipwa sh.3,000,000/=kwa ajili ya kusafirisha mwili na kwa majeruhi bima itatoa kiasi cha sh.500,000/=
"Real Insurance itatengeneza vibao maalum ambavyo vitakuwa na bendera maalumu ya nchi, gari linakokwenda na stika maalum inayoonesha kuwa limekatiwa bima ya dereva na atapewa namba za simu kwa ajili ya kupiga endapo atapata tatizo akiwa safarini ambapo namba hizo zitapatikana katika vituo vyote vya polisi vilivyoko katika barabara iendayo nchi za jirani," alihitimisha.
(PICHA / HABARI: NA DENIS MTIMA/GPL)